Ad Code

Agosti 19, 2022; Ijumaa: Juma La 20 La Mwaka

SOMO 1: Eze. 37: 1-14

Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana. Akaniambia, “Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi?” Nami nikajibu, “Ee Bwana Mungu, wajua wewe.” Akaniambia tena, “Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la Bwana. Bwana Mungu aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi. Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.” Basi nikatoa unabii kama nilivyoamriwa; hata nilipokuwa nikitoa unabii, palikuwa na mshindo mkuu; na tazama, tetemeko la nchi, na ile mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe. Nikatazama, kumbe! Kulikuwa na mishipa juu yake, nyama ikatokea juu yake, ngozi ikaifunika juu yake, lakini haikuwamo pumzi ndani yake. Ndipo akaniambia, “Tabiri, utabirie upepo, mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana Mungu asema hivi, ‘Njoo kutoka pande za pepo nne, Ee pumzi, ukawapulizie hawa waliouawa, wapate kuishi.”’ Basi nikatabiri kama alivyoniamuru; pumzi ikawaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno. Kisha akaniambia, “Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa.” Basi tabiri, uwaambie, “Bwana Mungu asema hivi; Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu, enyi watu wangu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo, na kuyatimiza.” Asema Bwana.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 107: 2-9

  1. Wasema hivi waliokombolewa na Bwana,
    Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi.
    Akawakusanya kutoka nchi zote,
    Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini.

(K)Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.
Kwa maana fadhili zake ni za milele.

  1. Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika;
    Hawakuona mji wa kukaa.
    Waliona njaa, waliona na kiu,
    Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao. (K)
  2. Wakamlilia Bwana katika dhiki zao,
    Akawaponya na shida zao.
    Akawaongoza kwa njia ya kunyoka,
    Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa. (K)
  3. Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake,
    Na maajabu yake kwa wanadamu.
    Maana hushibisha nafsi yenye shauku,
    Na nafsi yenye njaa huijaza mema. (K)

INJILI: Mt. 22:34-40

Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; “Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?” Akamwambia, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.”

TAFAKARI
MAPENDO KWA MUNGU NA JIRANI: Sarafu moja ya fedha na fedha ya noti moja daima huwa na pande mbili, lakini bado ni sarafu moja au noti moja. Na ili fedha hizo ziwe halali ni lazima pande zote mbili ziwepo. Na hivi ndivyo tunavyoalikwa na Yesu leo kuwa utimilifu wa maisha ya Mkristo huonekana katika kushika Amri Kuu ya Mapendo kwa Mungu na kwa jirani. Yesu anajumuisha amri na sheria zote katika Amri Kuu ya mapendo ambayo ina pande mbili, yaani mapendo kwa Mungu na Mapendo kwa jirani. Ni rahisi kukazia mapendo kwa Mungu, na kumchukia jirani ambaye katika maisha ya kila siku yuko karibu nawe. Mtume Yohane katika barua yake ya kwanza anatuasa “Mtu akisema, ‘Nampenda Mungu’, lakini anamchukia ndugu yake, ni mwongo. Kwa maana asiyempenda ndugu yake, ambaye anamwona, atawezaje kumpenda Mungu asiyemwona? Basi kwake tumepata amri hii: ampendaye Mungu ampende na ndugu yake.”’ (1 Yohane 4:20-21). Matendo na maneno yetu yote yaelekee katika kutimiza amri hii Kuu ya mapendo.

SALA: Ee Mungu, utujalie moyo wa kukupenda wewe daima na kuwapenda jirani zetu na kuwaombea.

Post a Comment

0 Comments