SOMO 1: Isa. 66:10-14
Furahini pamoja na Yerusalemu, shangilieni kwa ajili yake, ninyi nyote mmpendao; furahini pamoja naye kwa furaha, ninyi nyote mliao kwa ajili yake; mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake, mpate kukama, na kufurahiwa kwa wingi wa utukufu wake. Maana Bwana asema hivi, Tazama, nitamwelekezea Amani kama mto, na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho, nanyi mtapata kunyonya; mtabebwa; na juu ya magoti mtabembelezwa. Mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji, ndivyo nitakavyowafariji ninyi; nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu. Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi, na mifupa yenu itasitawi kama majani mabichi; na mkono wa Bwana utajulikana, uwaelekeao watumishi wake.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 66:1-7, 16, 20 (K) 1
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.
Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Imbeni utukufu wa jina lake.
Tukuzeni sifa zake,
Mwambieni Mungu, matendo yako yanatisha kama nini! (K)
Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
Naam, italiimbia jina lako.
Njoni yatazameni matendo ya Mungu,
Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu. (K)
Aligeuza bahari ikawa nchi kavu;
Katika mto walivuka kwa miguu;
Huko ndiko tulikomfurahia,
Atawala kwa uweza wake milele. (K)
Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
Na ahimidiwe Mungu aliyeyakataa maombi yangu,
Wala kuniondolea fadhili zake. (K)
SOMO 2: Gal. 6:14-18
Mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya. Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, Amani na iwe kwao rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.
SHANGILIO: Yn. 1:12, 14
Aleluya, aleluya,
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya.
INJILI: Lk. 10:1-12, 17-20
Baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenye kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni, angalieni, nawatuma kama wanakondoo kati ya mbwa-mwitu.
Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yoyote mtakayoingia, semeni kwanza, amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihamehame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wowote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia. Na mji wowote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yenu tunayakung’uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia. Nawaambia ya kwamba siku ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo.
Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.
TAFAKARI
Furahini kwa kuwa Majina yenu
yameandikwa Mbinguni
“Mpigieni Mungu kelele za shangwe nchi yote.” Hii ni Zaburi ya 66, Zaburi ya shukrani kumshukuru Mungu anayeokoa. Sisi nasi tumewahi kutendewa makubwa na Mwenyezi Mungu. Tusisahau kurudi kwake kwa shukrani na kutimiza ahadi zetu. Katika somo la kwanza, Nabii Isaya anatoa unabii wa amani na furaha kwa Israeli kwamba watashibishwa kwa maziwa ya faraja zake na watafurahia kwa wingi wa utukufu wake. Israeli anaahidiwa amani kama kijito kifurikacho. Huu ni ujumbe wa matumaini kwa Wayahudi waliotoka uhamishoni.
Walikuwa na mategemeo makubwa sana watakapofika Yerusalemu. Lakini cha ajabu, walikutana na kundi la wanaowachukia, waliokataa kuwakaribisha. Mwenyezi Mungu anawataka waondoe hofu; na wajitahidi waondokane na tamaa. Wamtegemee Mwenyezi Mungu na hakika Bwana atawabariki na kuwapatia amani. Wayahudi walishindwa kuiona amani ndani ya Yerusalem kwa sababu walikuwa na matarajio makubwa sana; hawakujua kwamba wao wenyewe walipaswa kunyanyuka na kuitengeneza amani kama mitume wanavyoambiwa na Yesu katika injili kwamba wawe vyombo vya amani. Sisi tuepuke kutegemea makubwa sana toka kwa wenzetu kwani wenzetu ni wanadamu na sio malaika. Hivyo, wakati wote anaweza kuanguka. Sisi tubakie kuwa watu wa bidii na kuepuka kuwa watu wa kufanya mambo kwa wastani. Tujiamini tukijua kwamba sisi wenyewe tunapaswa tuwe mstari wa mbele katika kutenda makubwa.
Katika injili, Bwana Yesu anawapatia maagizo wafuasi 70 na kuwatuma kuhubiri habari njema. Yesu anawatuma kama watumishi na sio kama mabwana. Anawataka pia wawe watu wa amani na kutii tamaduni mahalia. Mitume walirudi kwa furaha hasa kwa kufanikiwa kuwafukuza pepo wachafu. Yesu anawataka watamani furaha kubwa zaidi, furaha ya majina yao kuandikwa mbinguni kwani sio kila aitaye Bwana Bwana atakayefanikiwa kuingia katika ufalme wa mbinguni. Yesu hakuwataka wafuasi wake wachukue mfuko wa pesa kwa sababu tamaa ya mali ni kikwazo katika utume wa Bwana. Kuna urahisi wa utume kufunikwa na shughuli za kidunia. Hii ni hatari iliyokuwa tangu kipindi hicho. Pia kuhusu kukunguta mavumbi walipaswa kuepuka kulaani, kutoa vitisho au laana. Waheshimu mila na desturi za watu.
Bwana Yesu alimuona Shetani akishuka kama umeme. Hii inamaanisha nini? Lakini tumepewa mamlaka ya kumshinda. Shetani ana nguvu kwa aliye na wasiwasi bila imani. Vilevile wafuasi wanaonywa kwamba wasiwe watu wa kupuuzia na kutojali. Adhabu wanayotangaziwa watakaopuuzia ujumbe na mafundisho ya mitume ni kubwa kuliko iliyowapata watu wa Sodoma na Gomora. Kati yetu wapo wanaopuuzia ujumbe wa Injili. Yafaa tubadilike.
Sala: Bwana, kwa kupokea sakramenti kila wakati, nisaidie nipate kutembea katika mwanga wako, Amina.
-----------------------------------------------
0 Comments