Nabii Eliya alisimama, kama moto, hata na neno lake likawaka kama tanuru. Yeye alileta njaa juu yao, na kwa juhudi yake akawapunguzia hesabu yao; kwa neno la Bwana akazifunga mbingu, na mara tatu kutoka huko akatelemsha moto. Jinsi ulivyotisha kwa miujiza yako! Aliye mfano wako ataona fahari. Aliyekufa ulimfufua katika mauti, kutoka kuzimu, kwa neno la Bwana. Ukawashusha wafalme mpaka shimoni, na watu wateule vitandani mwao. Ukapaka mafuta wafalme kwa kisasi, na nabii ili akufuate nyuma yako. Ulisikia makaripio huko Sinai, na hukumu za kisasi huko Horebu. Ukachukuliwa juu katika kisulisuli, katika gari la farasi wa moto. Ukaandikiwa kuwa utaleta makemeo, ili kutuliza hasira siku ile ya Bwana; kugeuza moyo wa baba umwelekee mwana na kuhusisha kabila za Israeli. Bila shaka wamebarikiwa wale waliokuona kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana unaishi. Ndiye huyo Eliya aliyefunikwa kwa kisulisuli; hata na Elisha naye akajazwa roho yake; akazidisha ishara maradufu, na yale yaliyotoka kinywani mwake yalikuwa ya ajabu. Siku zake zote huyu pia hakushawishwa kwa kumwogopa mwenye kutawala, wala hakutiishwa na mtu ye yote. Hakukutokea neno lililokuwa gumu la kumshinda, hata na alipolala mautini mwili wake ulitoa unabii; kama alivyofanya miujiza katika maisha yake, kadhalika na katika mauti yake kazi zake zikawa za ajabu.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 97:1-7
- Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na virurahi.
Mawingu na giza vyakuzunguka,
Haki na hukumu ndio msingi wa kiti.
(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.
- Moto hutangulia mbele zake
Nao huwateketezatesi wake pande zote.
Umeme wake uliangaza ulimwengu,
Nchi ikaona ikatetemeka. (K) - Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana,
Mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zimetangaza khaki yake,
Na watu wote wameuona utukufu wake. (K) - Na waaibishwe wote waabuduo sanamu,
Wajivunao kwa vitu visivyofaa;
Enyi miungu yote, msujuduni Yeye. (K)
INJILI: Mt. 6:7-15
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.”
TAFAKARI
MSALIPO SALINI HIVI: Yoshua Bin Sira anatoa wasifu wa Nabii Eliya na matendo yake yaliyoendelezwa na Elisha aliyepokea roho na nguvu zake maradufu. Katika wasifu wa Eliya, msimulizi anataja mara tatu ‘moto’. Kwa Waebrania, Eliya aliwasilishwa kwa moto. Moto uliotumika kwenye sadaka za kuteketezwa, ili kuwaunganisha wanaoabudu na Mungu. Moto unatia joto, unaangazia, unatakasa na mara nyingine unaharibu. Yesu mwenyewe alisema amekuja kuwasha moto na alitamani kuona umewaka. Katika injili Yesu anawafundisha mitume wake kusali, namna ya agano jipya ya kuwasiliana na Mungu.
Sawa na moto wa sadaka za kuteketezwa ulivyotumiwa kuwaunganisha watu na Mungu, Kristo anatufundisha kuungana na Mungu mioyoni katika sala. Anatufundisha kumtambua Mungu kama Baba yetu, kutanguliza sifa za jina lake, na kujikabidhi kwenye mapenzi yake. Ndipo tunapomwomba mahitaji yetu ya msingi, msamaha na kumuomba atuopoe maovuni. Tunahimizwa kusamehe, ndipo tuombe na kupokea msamaha.
SALA: Baba Yetu …

0 Comments